MRADI WA KUSWAHILISHA PROGRAMU HURIA

 

 

WARSHA YA ARUSHA 1-5 NOVEMBA 2004-11-22

MADA YA MAFUNZO

 

 

UKUZAJI WA ISTILAHI: MISINGI YA KISARUFI

 

 

 

Zsm Mochiwa

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 


 

 

 

1.     UTANGULIZI

Kukua, kwa nafsi yake, ni kuongezeka nguvu, kimo, ukubwa, umri, n.k. Inaposemwa kuwa, lugha fulani inakua, ina maana inaongezeka uwezo wa kutekeleza majukumu yake; inapata nguvu za kimawasiliano katika kuratili (articulate) ulimwengu kwa usahihi zaidi. 

 

Kukua kwa Kiswahili, kwa mfano, huonekana kwa kuingia katika matumizi, maneno mapya au kutumika kwa maneno makuukuu kwa maana mpya. Kwa kadri miaka inavyopita Kiswahili hutoka katika kambi ya jumla jamala (generalities) na kuzidi kuwa na umahususi (specificity). Badala ya kuwa na neno moja, mguu, kwa mfano, lenye maana ya sehemu ya mwili kuanzia kiunoni hadi wayoni, kukua kwa Kiswahili kutaugawa mguu huo huo, uwe na kiweo/paja, kiga, muundi, futi, chafu, n.k.

 

Kukua ni miongoni mwa nduni (features) za kimaumbile za kitu cho chote kilicho hai.  Kwa kuwa hai, Kiswahili hupokea, kila uchao, maneno na/au vipengele mbali mbali vya lugha, mwafaka wa mahitaji mapya yanayozuka.  Uwezo huu wa Kiswahili wa kujipanga upya kwa kulingana na changamoto mpya, umo ndani ya maumbile yake.

 

 Siri hii ya maumbile ya lugha huwa mwega wa kauli mbili zinazotolewa mara kwa mara na wanaisimu (linguists).  Wataalam hao wanadai kuwa, nafsi ya lugha yoyote, imo katika sarufi yake. Hivi ni kusema, sarufi ndiyo inayoipa lugha ile dhati yake, yaani, ile nidhamu ya kuunda maneno yake, kuyapangilia na kuyatamka. Kwa kigezo hicho, Kiingereza, kwa mfano, ni mbali na Kiswahili.

 

  Hiyo mosi, lakini pili, kwa kigezo hiki cha sarufi, hakuna lugha yo yote iliyo ndogo au kubwa kuliko nyingine.  Kwa kigezo cha sarufi, Kiswahili na Kiingereza au lugha nyingine yoyote ni sawa. Kinyume cha hivyo, itakuwa vigumu Kiingereza kupata nafsi ya lugha kwa sababu, zaidi ya asilimia sabini ya maneno yake ni ya mkopo. Lakini kwa kuingizwa kwa maneno hayo ya kigeni katika nidhamu maalum, yaani ile sarufi yake, Kiingereza kimebakia na nafsi yake.

 

Maadam inakubalika kwamba zinakua, basi si muhali hata kidogo, kudai kuwa lugha yoyote hai itakuwa na mabadiliko kila uchao.  Mabadiliko hayo ndani ya maumbile ya lugha hutokea ama kwa polepole ama kinguvunguvu. Mabadiliko ya polepole ndiyo yaliyo ya kawaida katika uhai wa lugha. Ni  mabadiliko yanayoletwa na mtu mmoja mmoja katika shughuli za kila siku. 

 

Mtu mmoja, kwa mfano, akigundua kitu kipya katika utafiti wake,

hukipatia jina. Linapoingia kwa mara ya kwanza, jina lile huwa kipengele kipya cha msamiati. Katika biashara yake, mfanya biashara huleta bidhaa mpya na majina yake ambayo yatakuwa mapya katika lugha ya jumuia.

 

Mathalan, maneno redio au sukari au gari, yaliingia katika Kiswahili kutoka katika Kiingereza kwa jinsi hiyo.  Hata hivyo, kwa kuwa bidhaa hizi hazikuingia kwa siku moja, ni dhahiri kuwa maneno haya nayo, hayakuingia kwa siku moja.

 

 Maneno tunayoingiza katika Kiswahili hivi sasa kwa ajili ya Uswahilishaji wa teknolojia ya kompyuta, ni mfano hai wa mabadiliko ya kinguvunguvu. Tunataka Kiswahili kieleze kikamilifu teknolojia ya mawasiliano ya Kompyuta.  Tumepanga kuwa baada ya kipindi cha miezi mitatu, Kiswahili kiwe na maneno ya teknolojia hiyo yasiyopungua  1300. 

 

 Haya ni mabadiliko makubwa ambayo yatawapa changamoto watumiaji.  Kwa kuingia kwa muda mfupi kama huu, watumiaji hulazimika kujifunza maneno mengi kwa wakati mmoja. Kujifunza idadi kubwa ya maneno kama hii ni sawa na kujifunza upya, lugha ambayo waliijua.  Mabadiliko haya huwanyang’anya wazungumzaji ule umilisi (competence) wa lugha yao waliokuwa nao kabla ya zoezi hili.

 

Kutokana na kweli hii, zoezi hili halina budi kufuata, kwa kadri itakavyowezekana, ruwaza (patterns) za lugha yenyewe. Matumizi sahihi ya ruwaza za kifonolojia, kimofolojia, kisintaksia, kisemantiki, n.k. ndiyo yatakayosababisha matunda ya zoezi hili kupata mlahaka wa walengwa.     Litakapogagamiza mambo, zoezi hili linaweza kuleta athari za namna nyingi, lakini hapa nitataja mbili.

 

 Kwa upande mmoja, bidhaa zetu zinaweza zisinunulike. Hii ina maana kuwa, walengwa wa zoezi letu wanaweza kuona uzito wa kupokea maneno tutakayounda. Watakapoona ugeni ‘mnene’ wa kimatamshi au wa kimofolojia au wa kisintaksia, watasema: hicho si Kiswahili! Kutozizingatia ruwaza hizi ni kuwalazimisha walengwa wajifunze upya fonolojia, mofolojia, sintaksia ya lugha yao wenyewe. Haya si mabadiliko yanayokubalika kwa urahisi.

 

  Kwa upande mwingine zoezi hili linaweza kuingiza katika Kiswahili, ulemavu utakaopunguza kiwango cha ujifunzikaji (learnability) wa lugha hii.  Mathalan, tukisha kubali kuvuruga ruwaza za umoja/uwingi, tukatia katoto/vitoto, tunaingiza ugeni unaopunguza ujifunzikaji. Maana, mwega wa ujifunzikaji wa lugha yoyote ni zile ruwaza za desturi zilizomo. Zitakapoingia ruwaza nyingine, tena kwa wingi, tatizo la kupungua kwa ujifunzikaji na hata kukosa mlahaka (reception) huongezeka.  Tujipe fursa ya kuabiri baadhi ya ruwaza hizo ambazo hujenga misingi ya kisarufi.

 

2.      MISINGI YA KISARUFI

 

Kuizingatia misingi ya kisarufi ya lugha kwa karibu katika jitihada ya kupanua msamiati ni kuikuza lugha kwa kuitumia nafsi yake. Zinapotumika  ruwaza mbali mbali  zilizomo ndani yake, katika viwango mbali mbali vya  kifonolojia na kifonetiki, kimofolojia, kisintaksia na kisemantiki, lugha hukua kwa mujibu wa maumbile yake.  Katika makala hii, tutaelezea ruwaza za kimofolojia kwa undani baada ya kueleza kwa ufupi hizi ruwaza nyingine.

 

2.1            Kifonolojia na kifonetiki

 

Kimsingi, kila lugha ina mpangilio wa desturi wa sauti na matamshi yake.  Katika kiwango cha fonolojia, kuna mpangilio wa fonimu uliokubalika. Kwa makusudi yetu hapa, tuchukue fonimu kuwa sauti ndogo ambazo huwakilishwa na herufi hizi tunazotumia katika maandiko. Fonimu moja au mbili huunda silabi, kama vile, a, ba, ta, ka, n.k. Kila lugha hupangilia sauti zake kwa namna yake.  Mathalan, silabi zifuatazo huonekana kwa wingi katika Kiswahili:

 

1.       I                  mifano:       au, ua, aua

          KI                mifano:      kata, tuta, na, mama, nani, nini

          KKI             mifano        ndondo, mbumbumbu, ndumba

          KKKI           mifano:       mbwanda,  mbweu, shindwa

 

Aidha, katika Kiswahili, mfululizo wa KKKI hujengeka kwa sauti teule. Sauti ya kwanza katika silabi ya KKKI  huwa m au n, ya pili inakuwa b ikiwa imeanza m au d au g ikiwa ya kwanza ni n. Sauti ya tatu itakuwa w.  Kinyume cha utaratibu huu, silabi itakayotumia sauti nyingine haina mlahaka katika Kiswahili.

 

Aidha, ingawa kwa kawaida Kiswahili hutamkwa kwa jinsi kinavyoandikwa, lakini yako mazingira ambayo yanaonesha kuwa fonimu huathiriana. Hali hii, inajitokeza katika maneno kama vile mwili, kwenda, twende n.k.  Kwa msisitizo au kwa makusudi ya kuratili, maneno haya hupata yakatamkwa muili, kuenda, tuende, n.k.  Fikiria jinsi unavyotamka maneno yafuatayo :

 

2.     Mwambie         (kwa haraka)

 muambie        (kwa pole pole na kwa msisitizo)

kwenda           (kwa haraka)  

 kuenda           (kwa pole pole na kwa msisitizo)

 

Jambo la kukumbuka hapa ni kwamba, tunapounda neno, hatuna budi tukumbuke mpangilio wa sauti pamoja na matamshi ya sauti hizo. Aidha, jambo hili ni muhimu zaidi wakati wa kutohoa. Tunapotohoa neno la kigeni tunalipatia uenyeji wa matamshi katika Kiswahili. Namna bora ya kutohoa neno, ni mtohoaji kujifanya kana kwamba hajui ile lugha inayotoa neno linalotoholewa. Fikiria, microprocessor, kwa mfano, makorosesa linafidi mradi ? Wewe ungelitohoaje ?

 

2.2     Kisintaksia na Kisemantiki

 

Katika kiwango cha sintaksia, Kiswahili kina mpangilio wa kutangaza kitu cha kusifiwa kabla ya kukisifu.  Mwenendo huu huenda kinyume cha Kiingereza ambacho hupangilia sifa kwanza kabla ya kutaja kinachosifiwa.  Tuangalie mifano hii:

 

3.       Kiswahili :             MTOTO mzuri, mweusi wa Kinyamwezi

Kiingereza :           A good, black  Nyamwezi  CHILD.

 

2.3           Kimofolojia :

 

Katika kiwango hiki, tunakutana na maumbo ya maneno. Karibu kila neno katika Kiswahili, kama zilivyo lugha za Kibantu, lina sehemu zisizopungua mbili. Data inayofuata, kwa mfano, ina maneno yenye sehemu mbili.  Sehemu ya kwanza inataja idadi na nyingine inadhihirisha dhati au nafsi ya kitu kinachotajwa na neno.  Tuangalie maneno hayo :

 

4.       M-toto                    WA-toto

KI-tabu                  VI-tabu

JI-we                     MA-we

 

Katika mifano ya hapo juu, M- ina maana ya mmoja, KI – ina maana ya kimoja na JI – ina maana ya moja.  Hali kadhalika, ingawa kwa maumbo tofauti, lakini,  WA-, VI-, na MA huleta maana ya ‘zaidi ya moja’.  Baada ya kutangaza idadi kwa maumbo ya herufi kubwa, sehemu ya kila neno iliyobakia, yaani, -toto, -tabu, na -we hutangaza nafsi ya kitu chenye idadi iliyotanguliwa kutajwa.  Hivyo –toto ni child au children kutegemea idadi inayotangazwa mwanzoni.  Kimofolojia muundo wa nomino za Kiswahili hudhihirisha ruwaza hii.

 

         

5.

IDADI

DHATI

M

Toto

WA

Toto

KI

Tabu

VI

Tabu

JI

We

MA

We

 

         

Ruwaza hii si ya Kiswahili pekee, bali pia, hudhihirika katika lugha nyingine, hususan  za Kibantu.  Lakini ruwaza ya Kiingereza huenda kinyume cha hii ya Kiswahili kwa kuanza na dhati na kumalizia idadi, kama mifano hii ilivyo:

 

6       

DHATI

IDADI

boy

s

cat

s

house

s

 

Wakati mwingine, tunapounda istilahi, haiwezekani kuzingatia kwa karibu mpangilio huo wa maumbo. Hii inajitokeza zaidi katika maneno ya sayansi za maumbile, kama vile, kemia, fizikia, n.k. Kwa  mfano, tunapotohoa neno  Carbondioxide, tunalazimika kuchukua mpangilio usio wa Kiswahili. Tuchukue kuwa tunatohoa Carbon kuwa Kaboni, di kuwa mbili au maradufu na oxygen kuwa oksijeni. Mpangilio huu, bila  ya kubadilishwa unakifanya Kiswahili kipokee mpangilio mpya wa maumbo. Kwa kuwa ile di ni kiidadi cha oksijeni, kuchukua dioksaidi ni sawa na kuchukua mbili oksijeni badala ya oksijeni mbili. 

 

Ingawa istilahi za kisayansi zina ‘ukimataifa fulani, lakini kila mkuzaji ana wajibu wa kulinda, kwa kadri iwezekanavyo, upekee wa lugha inayopokea istilahi zake. Mkuzaji hana budi kulinda ruwaza kwa maana ya kuzitumia katika mchakato wa ukuzaji. Faida kubwa ya jitihadi hizi ni kuzifanya itilahi hizo zikubalike na ya pili ni kulinda ufunzikaji wa lugha yenyewe. Yanapozidi, maneno yanayokiuka mikondo ya kimaumbile hupoteza sifa zote mbili: ya mlahaka wa maneno yenyewe na ujifunzikaji wa lugha inayohusika.  

 

Uhai wa vitenzi vya lugha za Kibantu unajitokeza katika michakato ya aina mbili. Kwa upande mmoja vitenzi vya Kibantu hunyumbuka. Mzizi wa kitenzi cha Kibantu hupokea maumbo yanayokifanya kiwe kirefu.  Mzizi wa piga ni pig. Mzizi pig unaponyumbuliwa hutupatia vitenzi mbali mbali kama hivi:

 

7.       piga, pigana, pigia, pigiana, pigisha, pigishana, pigishania, n.k.

 

Vitenzi hivi vinachanuza maana moja ya msingi. Lakini kila kitenzi kinatofautika kidogo kimaana kutokana na kuongezeka kwa maumbo.Katika kunyumbuka kwake, pig imeongezewa –a, an-a, -I-a, -I-an-a, -ish-a, n.k. Kila umbo lililoingezwa limeandamana na mabadiliko ya maana. Mathalan, ingawa kitenzi pigana kinachukua maana ya piga lakini pigana inapangilia upya washiriki wa kitendo.   Kitenzi pigana kinatangaza watu wawili au zaidi wanaoshiriki kupiga, kila mmoja dhidi ya mwenziwe. 

 

Kweli hii ya kuongezeka kwa nguvu ya kimawasiliano kutokana na unyumbukaji wa vitenzi inadhihirika vizuri kwa kuangalia maisha ya -i/e-. Kutokea kwa – i/e – katika kitenzi piga kikapata sura ya  pigia, hutupatia nguvu ya kueleza maana nyingi:

 

8.       pigia           (a)      piga kwa ajili/niaba ya / dhidi ya mtu mwingine

(b)      tumia chombo X kwa kutekelezea kitendo

(c)      tumia sehemu Y katika kupiga        

                 (d)      piga X kwa sababu ya Y

 

Kinapofunguliwa kwa kutumia umbo la unyumbulishi – i/e - kitenzi kinapata uwezo wa kuhusisha watu au vitu katika utekelezaji wa kitendo cha msingi piga.  Pengine maana hizi mbalimbali zinaweza kupangiliwa hivi kwa kutumia kitenzi kingine PIKA.

 

9.       PIKIA:         (i)       Pika kwa ajili ya watoto          Pikia watoto (nani?)

                               (ii)     Pika kwa kutumia kuni          Pikia kuni (nini?)

 

                              (iii)     Pika ndani ya jiko = Pikia jikoni (wapi?)

                              (iv)    Pika kwa sababu ya taabu =     Pikia taabu (kisa)

 

Kinadharia, kila kitenzi kina uwezo wa kuingia katika unyumbulikaji unaozaa vitenzi vipya . Vitenzi hivyo huchanuza ruwaza  mahsusi ya maana.  Kwa kuitumia ruwaza hii, mtu anaweza kupata tafsiri za Kingereza hiki:

 

10.              Cook for someone

Cook with a stove

Cook in the kitchen

Cook because of/as a result of being forced by someone.

 

Mchakato huu wa unyumbulikaji hufungua pazia la kuzaliwa kwa nomino ambazo ni chanzo imara cha maneno mapya.  Mathalan, tuchukue kitenzi kingine PENDA. Kwa kunyumbulika kwake, kitenzi hutupatia:

 

11.     PENDANA, PENDEA, PENDEKA, PENDEKEA, PENDEKEZA, 

           PENDELEA, PENDEZA, PENDEZEA, PENDEZEANA, n.k.

 

Maneno haya yanayozaliwa hutupatia mwega wa mchakato wa pili ambao tutauita unominishaji. Huu ni mchakato unaotupatia nomino. Kinadharia, kila kitenzi kinachojitokeza kinaweza kunominishwa hivi:

 

12.     pendano, pendeo, pendeko, pendekeo, pendekezo, pendeleo, pendezo, pendezeo, pendezeano, n.k.

Ninasema kinadharia kwa sababu, si kila nomino inayoibuka ina matumizi hai. Nomino kama pendeo, pendeko, pendekeo, pendezo, pendezeo, pengine, mpaka sasa yana uhai katika ulimwengu wa ushairi zaidi kuliko kwingineko.  Lakini jambo la msingi ni kwamba hatuna sababu inayotuzuia tusiyaingize katika matumizi maneno hayo yanayozaliwa.

 

Aidha, ili tufaidi utajiri huu, inatubidi tuwe macho kuelewa vyema kiunzi cha kisemantiki (semantic frame) cha nomino hizi.  Katika kulifafanua suala hili, hatuna budi kuabiri baadhi ya vijenzi vya nomino.  Kwa makusudi hayo tuchunguze, bila ya kuvinyumbua, uhai wa vitenzi shinda, tuma, peta na panda.    

 

13.   shinda           -shindi,       -shindaji,    -shinde        ______________

        tuma              ___              -tumaji,        -tume          _______________

        peta               ____             -petaji,         -pete            -peto

        pinda                      -pindi,         -pindaji,      -pinde,        -pindo

 

Vijenzi vinavyotuletea mizizi ya nomino tuliyoiona hivi punde ni:

 

14.      -I                mfano         mshindi

           -E                                 mshinde

 

          - JI                                mpetaji

           - O                                pindo

 

Kila kijenzi kina maana mahsusi.   Tuangalie kimoja kimoja:

 

2.3.1    KIJENZI –I

 

Kijenzi -I hutuletea nomino kama vile: msomi, mjenzi, mvuvi, n.k.  Kila kinapotumika, kijenzi hiki hutangaza utaalamu, uzoevu wa kujihusisha na tendo linalofungamana na kitenzi. Msomi, kwa mfano, ni mtu aliyesoma jambo fulani kwa undani, mtaalamu mzoevu wa uwanja wa taaluma fulani.  Hali kadhalika, mvuvi ni mzoevu, mtaalam wa kuvua; hupata riziki zake kwa kazi hiyo. Hivyo nomino nyingi za Kiingereza zinazodokeza professionalism n.k. huweza kufasiriwa kwa nomino zenye kijenzi hiki.

 

15.    Fisherman                                mvuvi          (vua)

         builder/constructor                   mjenzi          (jenga)

         Orator                                       msemi          (sema)

         Lover                                                  mpenzi         (penda)

         Cook                                         mpishi          (pika)

         Hunter                                      msasi          (saka)

 

Kijenzi hiki kinajitokeza katika vitenzi ambavyo hutumika pamoja na maneno mengine yanayotaja vitu, watu, n.k. Mifano hai ya vitenzi hivyo

ni: pika ugali. suka nywele, penda watu, n.k. Vitenzi vya aina hii ndivyo vinavyotuletea nomino hizi zifuatazo:

 

16.     Mpishi (wa ugali), yaani,          mtu anayepika ugali

Msusi (wa nywele), yaani,        mtu anayesuka nywele

Mpenzi (wa watu), yaani,         mtu anayependa watu kwa dhati.

 

Nomino hizi kwa pamoja hutangaza ‘watenzi’ wa mambo. Mpenzi, kwa mfano hapendwi bali anapenda! Mtu anapodai kuwa fulani ni mpenzi wake ana maana kuwa huyo fulani ndiye anayempenda. Hivyo ni kusema, mtu huyo ni mpendwa wa huyo fulani ambaye ni mpenzi wake. Sasa tuangalie kijenzi –ji ambacho ki karibu na hiki tulichoona hivi punde.

 

2.3.2   Kijenzi –ji

 

Kijenzi hiki pia hutangaza ‘watenzi’ wa aina fulani. Tofauti kati ya kijenzi hiki na kile kingine imo katika uwezo, uzoevu, utaalamu, ung’ang’anizi, n.k. Mvuaji si mvuvi wa kila siku; mjengaji si mjenzi wa kila siku. Wote hawa huvua na kujenga kwa siku moja moja. Kwa kawaida, watu hawa hawapati riziki zao za kila siku kwa njia ya kuvua wala kujenga.

 

Katika kujenga, kwa mfano, mjenzi ana utaalam wa hakika pamoja na uzoevu na si ajabu ana vyeti kabisa. Aidha, anaponyang’anywa tenda za kujenga, si ajabu akawa amepoteza hata mzungu wa maisha yake kabisa. Mjengaji ni mtu wa kubabiababia tu. Hategemei kazi hiyo hyo tu. Yeye, aghalabu ya mambo ni mtu wa ‘kubangaiza’. Tuangalie mifano hii michache:

 

17.     Vuna           Mvunaji (ling. na mvuni)

          Choma        Mchomaji (ling. na mchomi)

          Chunga       Mchungaji (ling. na mchungi)

          Tenda         Mtendaji  (ling. na Mtenzi)

 

Kijenzi –ji kimestawi zaidi, pengine kuliko –I. Hali hii inaashiria kuwa utenzi wa mambo ni wa nadra zaidi ya utendaji. Watu wengi hufanya mambo kwa kupitia kuliko kuishia.  Hata hivyo, inafaa ikumbukwe hapa kwamba, kijenzi –ji hupata kikapewa hadhi sawa na kile cha –i. Mathalan, Mwenyekiti Mtendaji wa Shirika fulani, si wa siku moja moja; ni mtenzi hasa. Aidha, sahihi ya mambo ingekuwa aitwe Mwenyekiti Mtenzi! Tuabiri kijenzi –0

 

2.3.3.                        Kijenzi –O

 

Karibu vitenzi vyote hukitumia kijenzi hiki kwa kuzalia nomino zinazotangaza maana mbalimbali. Miongoni mwa maana hizi ni ile ya kile kinachotokea baada ya utenzi. Hii ina maana kuwa, ile nomino inayozaliwa inasema tunda la kitenzi chake. Tuangalie vitenzi vichache ili tulithibitishe dai hili:

 

 

18.     Ziba   zibo:  kitu kinachotumika katika mradi wa kuziba

          Futa   futo:   kitu kinachotumika katika mradi wa kufuta

          Pata  pato:  kitu ambacho mtu anapata

          Zaa   zao:   kitu ambacho kinazaliwa

          Peta   peto:  kitu kinachopatikana baada ya kupeta

 

Kila nomino ambayo ina kijenzi cha –O hutangaza moja kati ya mambo mawili. Ama inatangaza tunda. Mfano mmoja wa maana hiyo ni pato ambalo ni tunda la kupata. Pato hutangaza kupata kwenyewe. Maana hii inajitokeza pia katika maana ya zao. Zao ni tunda la kitendo cha kuzaa.

 

Wakati mwingine, nomino zinaweza kutangaza vifaa vya utekelezaji wa vitendo vinavyohusika. Tuchukue mfano wa kiZIBO. Kizibo ni kitu cha kutumia katika kuziba. Viko vitenzi vingi vyenye uwezo wa kuzaa nomino za aina hii. Tuangalie vitenzi hivi:

 

19.     Unda           Nyundo       kitu kinachotumika katika kuunda

          Tega           Mtego          kitu cha kutumia kwa ajili ya kutega

Kaga           Kago           kitu kinachokaga 

          Finga          Fingo           kitu kinachotumika kwa ajili ya kufinga   

 

 Kijenzi –O kinaweza kutangaza namna kitenzi kinavyoingizwa katika tendo. Maana ya mpigo, nomino inayotokana na kitenzi PIGA ni namna ya kupiga. Nguvu za kimawasiliano za kijenzi hiki hudhihirika hivi:

 

20.     mpigo                   namna ya kupiga

          mapigo        dharuba (marudio ya) za kupiga

          kipigo                   kitendo cha kupigwa

          Mzibo          namna ya kuziba

          Kizibo                   kifaa kinachoziba

          Mfuto          namna ya kufuta

          Mfuto          kitu cha kinachofuta

 

Kwa matumizi ya maombo mbali mbali ya idadi, inawezekana kutumia shina moja lanomino kama pigo kupata nomino zaidi ya moja. Mfano mzuri ni ule tulioona wa mpigo, mapigo na kipigo. Kila mjenzi wa istilahi aliye na hazina ya namna hii ya misingi ya kimofolojia atakuwa anaingiza maneno ambayo hayagunwi na walengwa. Aidha, maneno hayo huweza kupokewa bila ya kusita. Tuangalie kijenzi cha mwisho.

 

2.3.4   Kijenzi –E

 

Msingi wa kimaana wa kijenzi hiki hutaja kitu ‘kinachotenzwa’. Hapa pana mifano dhahiri:

 

21.     Mtume                  mtu aliyetumwa

          Upinde                  uliopindwa

          Upote                    uliopotwa

          Pete                      iliyopetwa

          Kiumbe                 kilichoumbwa

 

 

MWISHO.

 

Tulichoshughulikia kwa juu juu hapa ni michakato ya aina mbili. Kwanza, kuna mchakato ambao unazaa vitenzi kutokana na kunyumbuka kwa vitenzi vyenyewe. Pili, tumeonesha mchakato mwingine ambao hutupatia nomino. Kinadharia, vile vitenzi vinavyozaliwa katika mchakato wa kwanza, vinaweza kutumia vijenzi vilivyojadiliwa vikazaa nomino. Michakato miwili hii, inaweza kuelelezwa hivi:

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

e             *           *                       *              *             *             *              *

 

ji             *           *                       *             *              *             *              *

 

i              *           *                       *             *              *             *              *

 

o             *           *                       *             *              *             *              *

 


     Pend      ea        eka         ekea        ekeza     elea         eza             ezeana

  

 

 Matumizi ya misingi ya kisarufi katika ukuzaji wa istilahi husaidia kwa namna mbili. Kwa upande mmoja, misingi hii huongeza mlahaka wa maneno yanayozaliwa. Kwa upande mwingine, misingi hii hukipatia Kiswahili ukuaji wa kimaumbile.